IQNA

Jinai za Israel

Afrika Kusini yataka ICC imkamate Netanyahu kutokana na mauaji ya kimbari ya Gaza

10:42 - November 09, 2023
Habari ID: 3477867
PRETORIA (IQNA)-Afrika Kusini imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake makuu mjini The Hague (ICC) kuuwajibisha utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na vitendo vyake vya ukiukaji wa sheria za kimataifa wakati utawala huo ukiendelea kufanya jinai dhidi ya binadamu katika Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Naledi Pandor, alisema wakati wa hotuba yake kwenye Bunge la nchi hiyo siku ya Jumanne kwamba: "Mauaji ya watoto, wanawake na wazee yanayofanywa na Israel ni kitendo ambacho kinaiwajibisha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kutoa hati ya kukamatwa mara moja kwa watoa maamuzi muhimu akiwemo Netanyahu (waziri mkuu wa Israel, ambaye anahusika na ukiukaji wa sheria za kimataifa za uhalifu."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini pia ametoa wito wa kusitishwa mara moja mashambulizi ya Israel katika ardhi ya Palestina inayozingirwa ambayo yanaendelea tangu Oktoba 7.

Pandor amesema kuwa: "Hali hii haiwezi kuvumiliwa; ukatili huu haupaswi kukubaliwa. Ni lazima tuitishe usitishaji mashambulizi sasa kama wabunge wa Afrika Kusini."

Aidha amesema: "Kama Waafrika Kusini, tunahitaji kupaza sauti zetu na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti zifuatazo kukomesha mateso. Moja, usitishaji mapigano mara moja. Pili, kufunguliwa kwa korido za kibinadamu ili misaada na huduma zingine za kimsingi ziwafikie wote wanaohitaji."

Waziri wa Afrika Kusini pia amehimiza "mageuzi ya mfumo wa utawala wa kimataifa" ambao "utatoa ulinzi kwa watu walio hatarini zaidi."

Matamshi hayo yametolewa siku moja baada ya Afrika Kusini kuwaita nyumbani wanadiplomasia wake wote waliokuwa Israel.

Wito wa Pandor unafanana na ule wa Rais wa Algeria au waziri mkuu wa mamlaka ya Palestina. Siku ya Jumatatu, Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria aliitaka ICC kuchukua hatua ya kuiwajibisha Israel kwa jinai inazofanya dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Siku hiyo hiyo, Waziri Mkuu wa Palestina, Mohammad Shtayyeh, aliitaka ICC kutoa hati za kukamatwa maafisa wa Israel kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara katika Ukanda wa Gaza.

Jinai tangu Oktoba 7

Tangu Oktoba 7, utawala wa kibaguzi wa Israel umekuwa ukiendesha mauaji ya umati na ya kizazi dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza ambapo kufikia sasa umekwishaua bila huruma Wapalestina zaidi ya 10,500, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. Kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Palestina, kwa wastani Wapalestina 15 wanauawa huko Gaza katika kila saa moja, kutokana na mashambulizi hayo makali ya Israel.

Ripoti za Wizara ya Afya ya Palestina zinaonyesha kuwa, takriban watoto 160 wanauawa kila siku huko Ghaza katika mashambulizi ya Wazayuni. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Wizara ya Afya ya Gaza ilitangaza Jumanne mchana kwamba idadi ya mashahidi wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza ilikuwa imefikia 10,328, wakiwemo watoto 4,237 na wanawake 2719.

Pia, katika kipindi hicho, Wapalestina milioni moja na laki nne kati ya wakazi wote milioni mbili na laki tatu wa Gaza wamekimbia makazi yao na sasa wanaishi katika hali mbaya sana.

Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) huku likisema kuwa "kulindwa raia wakati wa migogoro sio matarajio au lengo bora tu, bali ni jukumu la pamoja la kibinadamu", limesisitiza juu ya "udharura wa kulindwa raia kila sehemu walipo.”

3485937

Habari zinazohusiana
captcha