IQNA

Jinai za Israel

Chile, Mexico zataka Mahakama ya Dunia ya Jinai, ICC, ichunguze jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

19:55 - January 19, 2024
Habari ID: 3478215
IQNA-Serikali za Mexico na Chile zimeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuchunguza na kuwashtaki maafisa wa utawala wa Israel ambao wamehusika katika jinai za kivita dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Mexico jana Alkhamisi ilisema katika taarifa kuwa, ICC ndio jukwaa bora la kuwawajibisha wahusika wa jinai dhidi ya Wapalestina wa Gaza; iwe ni maajenti wa Israel au maafisa wenyewe wa utawala huo haramu.

Mexico kwa upande wake imeashiria ripoti kadhaa za Umoja wa Mataifa zilizosema kwamba jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zimefanyika Gaza, na kwamba jinai hizo zinapasa kuchunguzwa na kusikilizwa na ICC.

Mapema mwezi huu, Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina, Francesca Albanese, na ripota maalum wa Umoja huo kuhusu haki ya makazi, Balakrishnan Rajagopal waliikosia vikali ICC kwa kutochukua hatua za haraka katika kuwashtaki maafisa wa utawala wa Israel ambao wamehusika katika jinai za kivita dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. 

Mwaka uliopita, Mexico ilichukua hatua ya kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Palestina, na sasa ofisi ya mahusiano ya Palestina katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini imepandishwa ngazi na kuwa ubalozi kamili.

Aidha mwishoni mwa mwaka uliopita, Rais wa Chile, Gabriel Boric alisema nchi hiyo inapanga kufungua ubalozi wake huko Palestina kwa shabaha ya kuongeza kiwango cha uwakilishwaji wake rasmi katika taifa hilo linalokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa muda mrefu sasa, aghalabu ya nchi za Amerikali ya Latini zimekuwa zikitangaza wazi wazi uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina, sambamba na kupinga sera kandamizi na jinai za Israel mkabala wa Wapalestina. 

3486866

 

Habari zinazohusiana
captcha