IQNA

Jinai za Israel

Vita dhidi ya Gaza: Israel yaendeleza mauaji ya kimbari, ubomoaji wa nyumba, hospitali na shule

14:26 - November 10, 2023
Habari ID: 3477873
GAZA (IQNA)- Kuendelea mashambulizi ya kila upande ya jeshi la Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza na kujiri mapigano makali kati ya vikosi vya muqawama na wavamizi hao karibu na kambi ya al-Shati iliyoko magharibi mwa mji wa Gaza, ni baadhi ya habari za hivi karibuni kutoka Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Katika siku ya 34 ya vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza, Wazayuni wameendelea kushambulia kwa mabomu na bila huruma maeneo ya makazi ya Gaza, ikiwa ni pamoja na nyumba, hospitali, shule na kambi za wakimbizi.

Katika taarifa yake jana asubuhi, Kamati ya Ufuatiliaji ya Makundi ya Wapalestina ilitahadharisha kuhusu kuongezeka majanga ya kibinadamu huko Gaza na kusema: "Gaza inakabiliwa na maafa makubwa."

Utawala wa Israel unaendelea kushambulia raia na hospitali katika mji wa Gaza bila kujali chochote, ambapo sehemu kubwa ya mji huo umeharibiwa kabisa. Mkurugenzi wa Hospitali ya Indonesia huko Gaza ameonya kuwa hospitali hiyo na maeneo jirani yanalengwa kwa makusudi na utawala wa Israel na kuwa umeme wa hospitali hiyo utakatika kabisa katika saa chache zijazo.

Utawala wa Kizayuni pia unaendelea kuishambulia kwa mabomu Hospitali ya al-Shifa. Moja ya vituo vya Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu katika mji wa Gaza, ambako misafara ya misaada ya kibinadamu imekuwa ikiratibiwa ili kufikishwa katika hospitali hiyo, kimeshambuliwa kwa mabomu na kuharibiwa kabisa.

Jumla ya hospitali 18 za Ukanda wa Gaza zimesitisha huduma zao kutokana na mashambulizi makali ya makombora na anga ya utawala wa Israel.

Msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP ameonya kuwa kuna changamoto kubwa ya uhaba wa chakula katika Ukanda wa Gaza kutokana na kusimama shughuli za vituo vya kuoka mikate, ambavyo ima vimeharibiwa katika mashambulio ya kinyama ya jeshi la Israel au vimekosa kabisa mafuta ya kuendeshea mitambo yao.

Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu, anasema: "Mauaji ya Gaza yanatoa changamoto kubwa kwa ubinadamu."

Tangu Oktoba 7, utawala wa kibaguzi wa Israel umekuwa ukiendesha mauaji ya umati na ya kizazi dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza ambapo kufikia sasa umekwishaua bila huruma Wapalestina zaidi ya 10,500, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. Kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Palestina, kwa wastani Wapalestina 15 wanauawa huko Gaza katika kila saa moja, kutokana na mashambulizi hayo makali ya Israel.

Ripoti za Wizara ya Afya ya Palestina zinaonyesha kuwa, takriban watoto 160 wanauawa kila siku huko Ghaza katika mashambulizi ya Wazayuni. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Wizara ya Afya ya Gaza ilitangaza Jumanne mchana kwamba idadi ya mashahidi wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza ilikuwa imefikia 10,328, wakiwemo watoto 4,237 na wanawake 2719.

Pia, katika kipindi hicho, Wapalestina milioni moja na laki nne kati ya wakazi wote milioni mbili na laki tatu wa Gaza wamekimbia makazi yao na sasa wanaishi katika hali mbaya sana.

Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) huku likisema kuwa "kulindwa raia wakati wa migogoro sio matarajio au lengo bora tu, bali ni jukumu la pamoja la kibinadamu", limesisitiza juu ya "udharura wa kulindwa raia kila sehemu walipo.”

Sambamba na kuendelea mashambulizi makali ya utawala wa Kizayuni katika mji wa Ghaza, vyanzo vya ndani vinaripoti kutokea mapigano makali kati ya wapiganaji wa muqawama na askari wa kigaidi wa Kizayuni katika maeneo ya kaskazini mwa mji huo.

Nguvu za kijeshi za wapiganaji wa muqawama wa Palestina zimepelekea kupungua kasi ya kusonga mbele jeshi la Israel au hata kusimama kabisa operesheni za jeshi hilo la adui katika baadhi ya sehemu.

Msemaji wa jeshi la utawala wa Kizayuni ametangaza kuwa: Tangu kuanza vita dhidi ya Ghaza, askari na maafisa 348 wa jeshi, polisi 59 na majasusi 10 wa Mossad wa utawala huo wameuawa katika mapigano na muqawama wa Palestina.

4180905

Habari zinazohusiana
captcha