IQNA

Jinai za Israel

Israel yaendeleza mauaji ya kimbari Gaza, idadi ya Wapalestina waliouawa yapindukia 7000

20:57 - October 27, 2023
Habari ID: 3477797
TEHRAN (IQNA)- Ofisi ya Habari ya serikali huko Gaza Palestina imetangaza kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi tangu utawala haramu wa Israel ulipoanza kufanya mashambulio mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7 imepindukia 7000 huku makumi ya maelfu ya wengine wakiwa wamejeruhiwa au kutoweka.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa, wengi wa mashahidi hao ni wanawake na watoto huku hali ya kibidamu katika Ukanda wa Gaza ikielezwa kuwa inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Takwimu hizo zinatolewa katika hali ambayo, duru mbalimbali za habari zimetangaza kuwa, mashambulio ya anga ya jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza yanngali yanaendelea.

Tangu kuanza kwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa siku 20 zilizopita sawa na Oktoba 7, kushambuliwa maeneo ya makazi na umma kwa upande mmoja na kukatwa maji, umeme na uhaba mkubwa wa chakula na dawa kwa upande mwingine, kumewafanya wakazi wa Ukanda wa Gaza kukabiliwa na hali ngumu sana na kupelekea taasisi za haki za binadamu kutangaza hali ya kibinadamu katika eneo hilo kuwa mbaya na ya kutisha. 

Hayo yanajiri katika hali ambayo, waungaji mkono wa wananchi wa Palestina katika maeneo mbalimbali ulimwenguni wameendelea kujitokeza na kuandamana wakilaani jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi wa Ukanda wa Gaza.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limeonya kuhusu tishio linalokabili maisha ya watu wa Gaza.

Wakati huo huo Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu imeonya kwamba, unga wa ngano katika Ukanda wa Gaza utaisha katika muda wa chini ya wiki moja.

Ashraf al-Qadara, msemaji wa Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, amesema mapema leo kwamba hawawezi tena kutoa huduma yoyote katika hospitali za Ukanda wa Gaza, na kwamba mfumo wa afya wa eneo hilo linalozingirwa na Israel unaporomoka kikamilifu.

Indhari ya Russia

Dmitry Medvedev Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia ametahadharisha kuwa, oparesheni ya nchi kavu ya Israel itafuatiwa na taathira nzito na za umwagaji damu.

Dmitry Medvedev leo Ijumaa ameandika katika mtandao wa Telegram kwamba: Msijidanganye. Oparesheni hiyo itaambatana na matokeo mabaya sana na umwagaji damu mkubwa. Medvedev ameendelea kuandika: Nchia za Magharibi zimeichoka sana Ukraine na sasa zinaiunga mkono Israel. 

Hamas yapondeza Russia na China

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amepongeza msimamo ulioonyeshwa na Russia na China katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hatua hayo ya kulipigia kura ya turufu azimio lililopendekezwa na Marekani la kuuunga mkono utawala vamizi wa Kizayuni unaokalia ardhi kwa mabavu.

Ismail Haniyah ameeleza katika taarifa maalumu aliyotoa, akizipongeza na kuzishukuru pia nchi zote wanachama na zisizo wanachama wa Baraza la Usalama ambazo zimetaka kusitishwa mara moja mashambulizi na jinai dhidi ya watu wa Gaza.
 
Aidha, Haniyah ameitaka Jamii ya Kimataifa iulazimishe utawala wa Kizayuni uheshimu haki za binadamu na kutekeleza sheria na maazimio ya kimataifa na ya kibinadamu kwa ajili ya haki za wananchi wa Palestina hususan watu wa Gaza.
 
Russia na China zimelipigia kura ya veto azimio lililopendekezwa na Marekani kuhusiana na Gaza katika Baraza la Usalama, ambalo lilikuwa linaupendelea utawala wa Kizayuni.
3485754
Habari zinazohusiana
captcha