IQNA

Sikukuu ya Idul Fitr

Ayatullah Khamenei: Israel "lazima iadhibiwe na kutiwa adabu" kwa kushambulia Ubalozi wa Iran

12:05 - April 10, 2024
Habari ID: 3478662
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei anasema utawala wa Kizayuni wa Israel "lazima uadhibiwe na kutiwa adabu" kwa shambulio lake baya dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria, Damascus.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo Jumatano katika hotuba za Swala ya Idul Fitr kwenye Uwanja Swala wa Mosalla Imam Khomeini katika mji mkuu wa Iran, Tehran, baada ya kuongoza Swala ya Idi inayoashiria kumalizika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Ayatullah Khamenei amesema, “Utawala mbovu wa Kizayuni ulifanya kosa jingine ... nalo ni shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria.

"Ofisi za ubalozi na za kidiplomasia katika nchi yoyote hutambuliwa kuwa eneo la nchi husika. Wanaposhambulia ubalozi wetu, ina maana wameshambulia ardhi yetu", amesema Sayyid Ali Khamenei.

"Utawala wa kishetani ulifanya makosa na lazima uadhibiwe na kutiwa adabu," amesisitiza Kiongozi Muadhamu.

Ayatullah Khamenei amelaani vita vya miezi kadhaa vya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa na kusema kuwa vinaonyesha uafiriti na sura mbaya ya ustaarabu wa Magharibi.

“Katika matukio ya mwaka huu, nchi za Magharibi zimeonyesha sura mbaya ya ustaarabu wa Magharibi. Katika kipindi cha miezi sita iliyopita huko Gaza, serikali za nchi za Magharibi, zenyewe, ziliweka wazi sura hiyo mbaya mbele ya macho ya ulimwengu. Wameua watoto waliokuwa wamepakatwa na mama zao na wagonjwa hospitalini. Wameshindwa kukabiliana na wanamapambano wa kambi ya Muqawama, hivyo wameamua kuua wazee, familia, watoto na wanawake, na kutoa roho za zaidi ya watu elfu thelathini wasio na hatia," amesema Kiongozi Muadhamu.

Katika sehemu moja ya hotuba zake za Swala ya Idi, Ayatullah Ali Khamenei amehoji: "Wako wapi wale ambao sauti yao kubwa kuhusu haki za binadamu inapasua masikio ya ulimwengu? Je, hawa (wanauawa huko Gaza) si wanadamu? Je, hawana haki yoyote?" 

Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba, kwa miaka mingi, serikali za nchi za Magharibi zimekuwa zikiisaidia na kuiunga mkono Israel, na pia zinaukingia kifua utawala huo katika duru za kimataifa na kuupa kila aina ya misaada.

Amesema, baadhi ya nchi hizo zinadai kuunga mkono watu wa Gaza, lakini kiutendaji zinashiriki katika vita vya Israel huko Gaza, hasa serikali zenye kiburi na katili za Marekani na Uingereza.” 

4209793

captcha