IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran

Mshiriki wa Saudia apongeza umaanawi katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran

14:45 - February 21, 2024
Habari ID: 3478389
IQNA - Mwakilishi wa Saudi Arabia katika Mashindano ya 40 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran amepongeza ubora na umaanawi au hali ya kiroho ya mashindano hayo.

"Imenibainikia kuwa mashindano hayo yamejaa umaanawi," Ustadh Abdul Qadir bin Marwan Saqaa ameliambia Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) katikla mahojiano pembezoni mwa mashindano hayo yanayomalizika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Tehran.

"Kuweka juhudi za kujifunza, kusoma na kuhifadhi Qur'ani Tukufu kunaonyesha jinsi tunavyothamini maneno ya Mwenyezi Mungu na jinsi kitabu hiki kitukufu kina maana kwetu sisi vijana na Waislamu wote," alisema.

Akizungumzia nafasi muhimu ya Qur'ani Tukufu katika kutafuta njia iliyonyooka, alisoma aya ya 9 ya Sura Al-Isra inayosema: “Hakika hii Qur'ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa, na inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo makubwa.”

Hafidh huyu wa Qur'ani Tukufu kutokaSaudi aliongeza, "Tunapoonyesha jinsi tunavyoijali Qur'an hii kama Waislamu, watu wengine wanaiheshimu zaidi kwa sababu Quran inatusaidia kuishi maisha bora."

Pia alipongeza kiwango cha juu na ubora wa washiriki na mashindano kwa ujumla.

Hii ni mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa kwa Saudi Arabia kutuma mwakilishi katika mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran. Siku ya Jumamosi, Balozi wa Saudia mjini Tehran Abdullah bin Saud al-Anzi alitembelea ukumbi wa mashindano hayo na ili kumtazamwa mwakilishi wan chi yake akiwa jukwaani.

Mashindano hayo ya kifahari yaliyoanza siku ya Alhamisi wiki iliyopita na yamewavutia wapenzi wa Qur'ani kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Zaidi ya nchi 110 zilikuwa na washiriki katika mashindano yam waka huu lakini ni washiriki 69 pekee kutoka nchi 40 waliofanikiwa kuingia katika duru ya mwisho baada ya mchakato mkali wa kuchujwa.

Washiriki wameshindana katika kategoria kuu za usomaji wa Qur'ani (kwa wanaume) na kuhifadhi Qur'ani na qiraa pamoja na Tarteel (kwa wanaume na wanawake).

Mashindano hayo yalimalizika jana  Jumanne, Februari 20, na washindi watatunukiwa katika hafla ya kufunga Jumatano ya leo katika hafla itakayoudhuriwa na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hafla hiyo ya kila mwaka inayoandaliwa na Jumuiya ya Masuala ya Wakfu na Misaada ya Iran inalenga kukuza utamaduni na maadili ya Qur'ani miongoni mwa Waislamu na kuonyesha vipaji vya wasomaji na wahifadhi Qur'ani.

3487276

Habari zinazohusiana
captcha