IQNA

Jinai dhidi ya Iran

Iran yawanasa magaidi 26 waliohusika na hujuma Shah Cheragh, Shiraz

20:41 - November 07, 2022
Habari ID: 3476053
TEHRAN (IQNA)- Wizara ya Intelijensia (Usalama) ya Iran imesema kuwa, vikosi vya usalama nchini vimewatia mbaroni magaidi 26 wakufurishaji ambao walihusika na shambulio la hivi karibuni la kigaidi kwenye Haram Takatifu ya Shah Cheragh katika mkoa wa kusini wa Fars na kuongeza kuwa, mratibu mkuu wa machafuko hayo hatari ni raia wa Jamhuri ya Azerbaijan.

Wizara hiyo, katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, ilitangaza kwamba ilianzisha operesheni kali za kiupelelezi mara baada ya shambulio hilo na kufanikiwa kuwatambua na kuwakamata wale wote waliohusika na kitendo hicho cha ugaidi cha umwagaji damu.

Taarifa hiyo ilisema kuwa waliokamatwa ni raia wa Jamhuri ya Azerbaijan, Tajikistan na Afghanistan, na hakuna hata mmoja kati yao ambaye ni raia wa Iran.

Imebainisha zaidi kuwa, gaidi ambaye alikuwa na jukumu kuu la kuratibu shambulio hilo la kigaidi ni raia wa Jamhuri ya Azerbaijan aliyeingia Iran kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini, Tehran, akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heydar Aliyev katika mji mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan, Baku.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mara moja alimfahamisha mshirika wake mmoja nchini Jamhuri ya Azerbaijan kuhusu kuwasili kwake mjini Tehran na kisha akawasiliana na mtandao wa wanachama wa kigeni wa kundi la kigaidi la Kitakfiri la Daesh nchini Afghanistan, linalojulikana pia kwa jina la Daesh katika Mkoa wa Khorasan, na kuwaambia kwamba yuko ndani ya Iran.

Taarifa hiyo iliendelea kubaini kuwa gaidi aliyetoa vifaa kwa ajili ya shambulizi la kigaidi huko Shiraz, ni raia wa Afghanistan aliyetambulika kwa jina la Mohammed Ramez Rashidi, anayejulikana zaidi kwa lakabu ya Abu Basir. Mpiga risasi katika hujuma hiyo alitambuliwa kama Sebahan Kamrouni, anayejulikana zaidi lakabu yake Abu Aisha, na ni raia wa Tajikistan.

Wizara ya Intelijensia ya Iran imesema magaidi hao wakufurishaji walitiwa mbaroni katika mkoa wa Tehran, mikoa ya kati ya Alborz na Qom na pia mikoa ya kusini ya Fars na Kerman pamoja na mkoa wa kaskazini mashariki wa Khorasan Razavi. Baadhi yao walikamatwa walipokuwa wakijaribu kutoroka Iran kupitia majirani wa mashariki.

Wizara hiyo imebaini kuwa baadhi ya wafungwa hao walikuwa wakipanga njama za kutekeleza vitendo zaidi vya ugaidi katika miji mingine ya Iran ukiwemo mji wa Zahedan kusini mashariki mwa nchi.

Ikumbukwe kuwa gaidi aliyekuwa na silaha nzito alivamia Haram Takatifu ya Shah Cheragh saa kumi na mbili kasorobo jioni  mnamo Oktoba 26, kabla ya sala ya Magharibi na kuua wafanyaziara 15 - ikiwa ni pamoja na mwanamke na watoto wawili - na kuwajeruhi wengine 40. Shah Cheragh ni Haram Takatifu na eneo la ziara alimozikwa Ahmad bin Musa Kazim SA, ambaye ni mwanae Imam Musa Kadhim AS, Imamu wa Saba wa Waislamu wa madhehebu ya Shia

Mshambulizi huyo alifyatua risasi kiholela akiwalenga waumini waliokuwa ndani ya haram hiyo takatifu. Aidha gaidi hiyo alijeruhiwa na maafisa wa usalama waliofika hapo haraka na aliangamia baadaye wakati akipata matibabu hospitalini.

Muda mfupi baadaye, kundi la kigaidi la Daesh lilidai kuhusika na kitendo hicho cha kigaidi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei na maafisa wengine wa Iran wametoa salamu za rambirambi kwa taifa la Iran na kutoa hakikisho kwamba wahusika wa jinai hiyo ya "kuchukiza" bila shaka watakabiliwa na adhabu.

4097712

captcha