IQNA

Ugaidi dhidi ya raia

Watu 15 wauawa katika hujuma ya kigaidi katika eneo la Shah Cheragh nchini Iran

22:20 - October 26, 2022
Habari ID: 3475990
TEHRAN (IQNA)- Zaidi ya watu 15 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya gaidi aliyekuwa na silaha nzito kushambulia eneo takatifu katika mkoa wa kusini magharibi mwa Iran wa Fars siku ya Jumatano.

Esmail Mohebbi-Pour, naibu mkurugenzi wa siasa, usalama, na masuala ya kijamii katika ofisi ya gavana wa jimbo la Fars amesema idadi ya waliofariki ni 15.

Taarifa zinasema watu wengine 40 walijeruhiwa katika shambulio hilo kwenye eneo takatifu la Shah Cheragh huko Shiraz, eneo la ziara alimozikwa Ahmad bin Musa Kazim, ambaye ni mwanae Imam Musa Kadhim AS, Imamu wa Saba wa Waislamu wa madhehebu ya Shia

Akitoa maelezo kuhusu shambulio hilo lililotokea Jumatano jioni, kamanda wa polisi wa jimbo la Fars alisema mshambuliaji pekee alifyatua risasi kiholela kwa wafanyaziara waliokuwa ndani ya haram hiyo takatifu na yeye mwenyewe alijeruhiwa na kukamatwa na maafisa wa usalama.

Duru zinadokeza kuwa, gaidi aliyetekeleza  shambulio hilo alikuwa raia wa kigeni.

Shirika rasmi la habari la Iran IRNA limesema watoto wawili na mwanamke mmoja ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo la kigaidi.

Wakati huohuo, mmoja wa mashuhuda wa shambulio hilo aliwaambia waandishi wa habari kuwa vilio vikali vilisikika katika sehemu ya wanawake ya eneo hilo wakati wa adhana na ghafla mtu mwenye silaha alionekana akiwa na bunduki aina ya Kalashnikov akifyatua risasi kiholela.

Baada ya ufyatuaji risasi wa awali, mshambuliaji alienda karibu na walipokuwa watu na kuwafyatulia risasi nyingi waliokuwepo kwenye eneo la tukio.

Gavana wa jimbo la Fars alinukuliwa akisema kwamba gaidi huyo kwanza alimlenga mtumishi na mlinzi wa eneo hilo takatifu, na alikusudia kuwashambulia waumini wakati wa Sala jamaa, lakini mmoja wa watumishi alimzuia kuingia kisha akaanza kufyatua risasi kiholela.

/4094747

captcha