IQNA

Jinai za Israel

OIC yaitisha mkutano wa dharura baada ya Israel kuvamia Msikiti wa al-Aqsa

9:57 - April 07, 2023
Habari ID: 3476827
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeitisha mkutano wa dharura kujadili hali ilivyo katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, baada ya askari wa utawala haramu wa Israel kuvamia Msikiti wa al-Aqsa mjini Quds (Jerusalem) na kuwalenga waumini wa Kipalestina kwa guruneti.

Sekretarieti Kuu ya OIC ilisema itafanya kikao cha dharura na cha wazi cha Kamati ya Utendaji katika ngazi ya Wawakilishi wa Kudumu, siku ya Jumamosi kwenye makao makuu ya Sekretarieti Kuu huko Jeddah, Saudi Arabia, kujadili uvamizi na mashambulio yanayofanywa na wanajeshi wa Israel dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa na waumini.

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi kutoa wito wa kufanyika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kujadili yanayojiri Palestina.

Wakati wa mazungumzo ya simu na mwenzake wa Indonesia Joko Widodo siku ya Alhamisi, Raisi alilitaka OIC yenye wanachama 57 kuitisha mkutano wa dharura ili kufikia uamuzi wa pamoja wa jinsi ya kutetea haki za Wapalestina wasio na hatia na kukabiliana na uhalifu wa utawala katili wa Israel.

Rais wa Iran ameitaja Palestina kuwa moyo wa ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza kuwa, "uungaji mkono wa haki za taifa la Palestina na mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni ni kanuni ya msingi ya Umma wa Kiislamu."

Ameongeza kuwa, umoja wa ulimwengu wa Kiislamu bado ni jambo la lazima ili kukabiliana na uchokozi na jinai za utawala wa Kizayuni.

Rais wa Iran alibainisha kuwa ulimwengu wa Kiislamu, kama kambi yenye ushawishi katika miligano ya kimataifa, unahitaji ushirikiano zaidi.

Widodo, kwa upande wake, alikaribisha wito wa mwenzake wa Iran wa mkutano wa dharura wa OIC kuhusu Palestina, akitumai kuwa tukio hilo linaweza kukuza zaidi uhusiano kati ya mataifa ya Kiislamu.

Siku ya Jumatano, vikosi vya Israel vilivamia eneo hilo takatifu kwa mara ya pili mfululizo na kujaribu kuwahamisha waumini wa Kipalestina kwa kurusha maguruneti na risasi za mpira.

Kulingana na Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina, takriban watu sita walijeruhiwa katika hujuma hiyo mpya.

4131945

captcha