IQNA

Benedict XVI, kiongozi wa zamani wa Kanisa Katoliki afariki

19:29 - December 31, 2022
Habari ID: 3476335
TEHRAN (IQNA)- Aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Benedict wa 16, amefariki dunia leo Jumamosi, akiwa na umri wa miaka 95.

Kifo chake kimetukia siku chache baada ya uongozi wa kanisa hilo mjini Vatican kutangaza kuwa kiongozi huyo wa zamani anaumwa na hali yake afya ni mbaya.

Taarifa kutoka Vatican zimesema, Papa huyo mstaafu aliyezaliwa nchini Ujerumani, na jina lake halisi ni Joseph Ratzinger, amefariki dunia saa tatu na dakika 34 asubuhi muda wa Vatican, kwa mujibu wa Matteo Bruni msemaji wa Vatican.

Papa Benedict wa 16, aliingia katika vitabu vya historia baada ya mwaka baada ya kujiuzulu upapa hapo wmaka 2013 na kuwa Kiongozi wa Kwanza wa Kanisa Katoliki duniani kuachia nafasi hiyo baada ya miaka 600, kwa kile alichokisema ni umri wake mkubwa na kuanza kudhoofika kwa afya yake.

Papa Benedict aliongoza Kanisa Katoliki kwa muda usiozidi miaka minane hadi mwaka 2013.

Aliondoka madarakani wakati Kanisa hilo lilipokuwa linakabiliwa na kashfa ya makasisi wake kuhusishwa na vitendo vya unyanyasaji wa kingono hasa dhidi ya watoto wadogo.

Benedict XVI aliwahi kutuhumiwa kwamba alififiliza na kuzembea katika kuchunguza matukio manne ya ripoti kuhusu ubakaji na unyanyasaji wa kingono waliofanyiwa watoto wadogo wakati yeye alipokuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Munich nchini Ujerumani.

Papa Benedict XVI alikuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Munich, Ujerumani kuanzia mwaka 1977 hadi 1982.

Katika kipindi hicho, kiongozi huyo alikataa kufanya chochote kuhusiana na unyanyasaji wa kingono waliofanyiwa watoto wadogo wanne na makasisi wa kanisa katoliki.

Ripoti iliyotolewa kuhusu kadhia hiyo imeeleza pia kwamba, akiwa na uelewa kamili, Papa Benedict XVI aliwaruhusu waendelee kufanya kazi kanisani, makasisii watatu ambao walithbitika kuhusika na vitendo hivyo.

Misimamo ya Benedict XVI

Papa Benedict XVI alijulikana kwa misimamo yake mikali. Ingawa alitangaza mara tu baada ya kutawazwa kuwa atafanya kazi ya kuunganisha pamoja makundi tofauti ya Wakristo na kuanzisha mazungumzo baina ya dini mbalimbali, lakini kauli zake kuhusu Uislamu zilizua wimbi la hasira katika baina ya Waislamu kote duniani.

Tarehe 12 Septemba 2006 Papa Benedict alitoa hotuba nchini Ujerumani, ambapo alinukuu maandishi ya kale yanayosema kuwa "Uislamu umekuja tu na mambo maovu na yasiyo ya kibinadamu". Matamshi hayo ya kongozi wa zamani wa Kanisa Katopliki yalizua wimbi la maandamano katika ulimwengu wa Kiislamu.

Joseph Aloisius Ratzinger alichagulikuwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki akiwa na umri wa miaka 78, baada ya kifo cha mtangulizi wake, Papa John Paul wa pili, mwezi Aprili mwaka 2005.

3481883

captcha