IQNA

Utawala wa Israel wawakatia maji Wapalestina katika Mwezi wa Ramadhani

15:07 - June 16, 2016
Habari ID: 3470391
Utawala wa Kizayuni wa Israel umewakatia huduma za maji Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan licha ya joto kali na hitajio kubwa la bidhaa hiyo muhimu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Ayman Rabi, Mkurugenzi Mkuu wa Kundi la Wasomi wa Sayansi ya Maji (Hydrology Group) huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu amesema maeneo mengi ya kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi yamekatiwa maji katika muda wa siku 40 zilizopita. Amesema maeneo yaliyoathiriwa zaidi na hatua hiyo ni manispaa ya Jenin, vijiji vya Nablus na mji wa Salfit. Ayman Rabi amesema familia nyingi katika Ukingo wa Magharibi zinalazimika kununua bidhaa hiyo muhimu kutoka kwa wachuuzi kwa gharama za juu. Mkurugenzi Mkuu wa Kundi la Wasomi wa Sayansi ya Maji huko Palestina ameongeza kuwa, familia moja inalazimika kutumia kati ya lita 2 hadi 10 za maji kwa siku licha ya kuwa na mahitaji mengi ya bidhaa hiyo. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mtu mmoja kwa wastani anafaa kunywa lita 7 na nusu za maji kwa siku.

Ragheb Al Haj Hassan, Meya wa mji wa Jenin amesema huduma hiyo muhimu imekatwa ghafla pasina kutolewa ilani na kusisitiza kuwa Waislamu wengi wa Palestina wanahangaika kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo haswa katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani.

3460097

captcha