IQNA

Mauaji ya Waislamu Nigeria kuchunguzwa

0:14 - May 01, 2016
Habari ID: 3470280
Mahakama ya Nigeria imeunda tuma ya uchunguzi kuhusu mauaji yaliyofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu Desemba 2015.
Tume hiyo ya mahakama itaanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya kutisha yaliyofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu wa mji wa Zaria katija jimbo la Kaduna kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Uchunguzi huo utaanza katika hali ambayo wiki iliyopita mashuhuda waligundua kaburi la umati ambalo ndani yake ilizikwa miili 350 ya Waislamu hao. Afisa mmoja wa tume hiyo ya uchunguzi amenukuliwa akisema kuwa, baada ya umwagaji damu mkubwa uliofanywa na jeshi hilo, liliamua kuizika miili ya wahanga katika kaburi hilo la umati. Amesema ushahidi unaonyesha kwamba, kwa akali watu 350 waliuawa katika hujuma ya tarehe 12 mwezi Disemba mwaka jana mjini Zaria, kaskazini mwa nchi hiyo. Afisa huyo ameweka wazi kwamba, siku moja baada ya mauaji hayo, mtu mmoja asiyejulikana alimpigia simu na kumtaarifu juu ya kuwepo kaburi la umati katika jimbo la Kaduna. Hii ni katika hali ambayo, Harakati ya Kiislamu nchini humo, imetaka kuwekwa wazi jinai iliyofanywa na askari wa serikali dhidi ya Waislamu katika tukio la mauaji ya Zaria. Aminu Abubakar, mmoja wa wajumbe wa harakati hiyo hapo jana Ijumaa sanjari na kulituhumu jeshi la nchi hiyo kwa kuhusika na mauaji dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo mjini Zaria, ametaka kufukuliwa miili ya wahanga wa mauaji hayo kutoka kwenye kaburi hilo la umati mjini Kaduna. Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita, Harakati ya Kiislamu ilifanya maandamano makubwa kwenda kwenye kaburi hilo. Wiki iliyopita pia Shirika la Msamahama Duniani la Amnesty International lililituhumu jeshi la Nigeria kwa kuwaua makusudi wafuasi wa harakati hiyo eneo lililotajwa ambalo lipo umbali wa kilometa 80 jimboni Kaduna. Shirika hilo lilibainisha kwamba aghlabu ya ushahidi wa jinai za Zaria uliharibiwa na jeshi hilo, ikiwa ni pamoja na kuharibu kabisa kituo cha kidini cha harakati hiyo ya Kiislamu na kadhalika makazi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi mkuu wa harakati hiyo. Amnesty International iliongeza kuwa, madai ya jeshi la nchi hiyo kwamba wafuasi wa harakati hiyo walikusudia kumuua kamanda mkuu wa jeshi la Nigeria mjini Zaria, hayana msingi wowote na ni ya kubuni tu. Kufuatia ripoti hiyo ya Shirika la Msamaha Duniani, Sani Osman, msemaji wa jeshi hilo ameitaja ripoti hiyo kuwa ya pupa na isiyo na itibari. Hata hivyo ukweli ni kwamba, kutolewa ripoti hiyo inaweza kuwa sababu ya kuadhibiwa wahusika wa jinai hiyo na kulipwa fidia familia za wahanga wake. Itakumbukwa kuwa, tarehe 14 mwezi Disemba mwaka jana jeshi la Nigeria baada ya siku moja ya kufanya mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu hao, liliizika kwa siri miili ya wahanga katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Muhammadu Mustafa, mjumbe wa harakati hiyo ya Kiislamu nchini Nigeria amesema kuwa, serikali ya eneo katika jimbo la Kaduna, inadai kuwa watu waliozikwa katika kaburi hilo la umati ni 347, katika hali ambayo idadi halisi ya mauaji hayo inapindukia idadi hiyo. Wito wa kutaka wahusika wa hujuma dhidi ya Husseiniyyah ya Waislamu hao waadhibiwe, unatolewa katika hali ambayo maafisa wa Shirika la Msamaha Duniani Amnesty International wamesema kuwa, hadi sasa idadi kubwa ya Waislamu bado wanaendelea kushikiliwa katika korokoro za jeshi la nchi hiyo huku wengine wakiwa hawajulikani waliko. Wakati huo huo baadhi ya duru za habari zimeripoti kwamba, jicho la kushoto la Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa harakati hiyo ya Kiislamu halioni huku mkono wake wa kushoto pia ukielekea kupooza. Aidha hali ya kimwili ya mke wake nayo inasemekana kuendelea kuwa mbaya siku hadi siku.
3493164
captcha