IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ukoo Khabithi, Uliolaaniwa wa Aal Saud Haustahiki Kusimamia Maeneo Mawili Matakatifu

22:47 - September 07, 2016
Habari ID: 3470552
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema utawala khabithi wa ukoo wa Aal Saud haustahiki kusimamia Haram Mbili Takatifu za Waislamu.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo asubuhi (Jumatano) mjini Tehran aliponana na familia za mashahidi wa Mina na wa Msikiti Mtakatifu wa Makkah. Aliongeza kuwa, kutokuwa na uwezo ukoo wa Aal Saud wa kusimamia Hija kulikopelekea kutokea matukio hayo mawili ya kusikitisha mwaka jana katika msimu wa Hija, kwa mara nyingine tena kumethibitisha namna mti huo khabithi uliolaaniwa usivyo na ustahiki wa kusimamia na kuendesha Haram Mbili Tukufu za Makkah na Madina. Amesisitiza kuwa: Kama Aal Saud wanasema kweli ya kwamba hawakuwa na makossa katika tukio hilo, basi waruhusu kuundwe tume ya kutafuta ukweli ya Kiislamu na kimataifa, ili iweze kuchunguza kwa karibu jambo hilo na kuwaonesha walimwengu uhakika wake.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, kuonana familia za mashahidi wa Mina na wa Masjidul Haram kunakumbushia tukio chungu la mwaka jana na kuongeza kuwa: Tukio la Mina lililopelekea kupoteza maisha mahujaji wengi wakiwemo wa Kiirani wakiwa katika ibada na katika midomo yenye kiu, chini ya jua kali, ni tukio la kusikitisha mno ambalo si rahisi kusahaulika. Tab'an tukio hilo lina vipengee mbali mbali vya kuweza kutumiwa kuwaamsha watu kisiasa, kijamii, kimaadili na kidini na inabidi vipengee hivyo visisahauliwe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema: Lilikuwa ni jambo zito sana kwa familia za mahujaji kusikia habari ya kufariki dunia wapendwa wao na kupokea maiti za jamaa za hao mwaka jana, lakini katika upande wa pili wa msiba huo, kuna jambo jengine nalo ni kujua kwamba, wapendwa hao ni sawa na mashahidi walioko chini ya kivuli cha maghufira, rehema na neema za Mwenyezi Mungu na hilo linazipa utulivu na kuzifariji nyoyo za wafiwa.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria kuuawa shahidi karibu mahujaji elfu saba mwaka jana katika maafa ya Mina na kutoa lawama kali akisema, kwa nini nchi na tawala zilizopoteza watu wao katika tukio hilo, hazioneshi radiamali yoyote?
Amesema, hatua ya viongozi wa nchi na maulamaa na wanaharakati wa kisiasa na wasomi na watu wenye vipawa katika ulimwengu wa Kiislamu kunyamazia kimya suala la kuuawa shahidi mahujaji elfu saba wasio na hatia, ni mtihani mkubwa kwa umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Kutoguswa na kutoonesha hisia zozote mbele ya maafa mazito na yaliyosababisha huzuni kubwa kama ya Mina, ni msiba mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, kitendo cha watawala wa Kisaudi cha kukataa hata kuomba radhi kwa maneno tu ni jeuri iliyopindukia mipaka na ni kukosa kwao haya na kuongeza kuwa: Hata kama tujaalie tukio hilo halikufanyika kwa makusudi, lakini wa kulaumiwa kwa kosa hilo ni kundi la watawala wa kisiasa wa nchi hiyo ambao wameshindwa kuweka mipango madhubuti ya kusimamia vizuri amali ya Hija.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake mbele ya majimui ya familia zenye majonzi za mashahidi wa Mina kwa kuuliza swali muhimu akisema: Wakati utawala fulani unaposhindwa hata kuwasimamia wageni wa Mwenyezi Mungu ambao kwenda kwao Hija kuna pato zuri kwa utawala huo, kuna dhamana gani ya kutojikariri maafa kama ya Mina wakati inapotokezea hali kama ya huko nyuma?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Taifa la Iran limesimama kishujaa kukabiliana na ujahili na upotofu wa ukoo wa Aal Saud na linaendelea kubainisha kwa uwazi misimamo yake ya haki inayotiwa nguvu na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na inabidi mataifa na nchi nyingine duniani zisimame kishujaa kukabiliana na ukoo huo wa Aal Saud.
Amesema, kushindwa Wasaudia kusimamia vizuri amali ya Hija na ukosefu wa usalama wanaobebeshwa mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah kwa hakika ni jambo linaloonesha kuwa utawala huo wa Aal Saud hauna ustahiki wa kusimamia Haram Mbili Tukufu na inabidi uhakika huo uenezwe na kubainishwa vilivyo katika ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, kipengee kingine kinachohusiana na tukio la Mina, ni kimya cha kutisha kilichoonesha na watu wanaodai kulinda haki za binadamu duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia makelele ya kisiasa na kipropaganda ya mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu kuhusiana na utekelezaji wa baadhi ya maamuzi ya mahakama katika baadhi ya nchi na kuongeza kuwa: Kunyamazia kimya tena vibaya sana uzembe wa utawala fulani ulioshindwa kutekeleza vizuri majukumu yake na kupekekea watu elfu saba kufa kidhulma tena bila ya hatia, kunazidi kudhibitisha uongo wa watu hao wanaodai kutetea haki za binadamu duniani na kwamba wale watu ambao wana tamaa na mashirika ya kimataifa kama hayo, wanapaswa kupata funzo kutoka katika tukio hilo chungu.
Ayhatullah Udhma Khamenei amesema, kuundwa tume ya kutafuta ukweli ni miongoni mwa kazi za wajibu na za dharura zinazopaswa kufanywa na nchi za Kiislamu na wale wanaodai kutetea haki za binadamu duniani. Ameongeza kuwa, baada ya kupita mwaka mzima tangu lilipotokea tukio hilo la kuhuzunisha mno, utafiti uliofanywa kuhusu nyaraka na ushahidi mbali mbali wa video, sauti na maandishi, umefichua kwa kiwango kikubwa uhakika wa tukio hilo.
Vile vile amewahimiza viongozi wa Iran kulipa uzito mkubwa suala kufuatilia uundwaji wa kama ya kutafuta ukweli na kuongeza kuwa: Kama Aal Saud wana yakini na madai kuwa hawana makosa katika tukio la Mina, basi wasifumbe midomo ya watu kwa kuwahonga fedha, na waruhusu kuundwa tume ya kutafuta ukweli ili kulichunguza kwa uhuru na kwa karibu suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwamba wanaouunga mkono utawala wa Aal Saud ni washiriki wa jinai za utawala huo katika maafa ya Mina na kuongeza kuwa: Utawala usio na huruma wa Aal Saud kwa uungaji mkono wa Marekani, umesimama kukabiliana na Waislamu kwa jeuri kubwa na unamwaga damu za Waislamu katika nchi za Yemen, Syria, Iraq na Bahrain, hivyo Marekani na waungaji mkono wote wa Riyadh ni washiriki wa jinai za Aal Saud.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia namna mashirika ya kipropaganda ya vibaraka wa Saudia yanayofanya kila njia kujaribu kuzihusisha jinai za Mina na hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni au ugomvi baina ya Waarabu na wasio Waarabu na kuongeza kuwa: Wanaowasaidia watawala wa Saudi Arabia katika propaganda wanakariri-kariri na kurudia-rudia madai ya uongo wakati ambapo wengi wa mahujaji elfu saba waliouawa shahidi huko Mina, ni Waislamu wa Kisuni licha ya kuweko pia mahujaji wengi wa Iran waliouawa shahidi kwenye maafa hayo.
Amesema: Ukoo wa Aal Saud na magenge ya magaidi makatili yalioanzishwa na kutiwa nguvu na wao wenyewe yanawaua kwa umati Waarabu katika nchi za Yemen, Syria na Iraq, hivyo tofauti na propaganda za kikhabithi zinazoenezwa na Wamagharibi, Wasaudia si watetezi na wala si walinzi wa Waarabu na kwamba tukio la Mina halina uhusiano wowote na mvutano wa kupandikiza unaodaiwa kuwepo baina ya Waarabu na wasio Waarabu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Uhakika wa jambo hilo ni kwamba, Wasaudia wanaochukiza, ni kundi ndani ya ulimwengu wa Kiislamu ambalo baadhi yao kwa kujua na baadhi yao kwa kutojua, wanawafanyia vitendo vya kiadui Waislamu na kwamba ulimwengu wa Kiislamu una wajibu wa kusimama kidete kukabiliana nao na vile vile utangaze kujibari na kuwa mbali kwake na mabwana wa Wasaudia yaani Marekani na Uingereza makhabithi.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amezitaka taasisi na vyombo mbali mbali nchini Iran ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje, Taasisi ya Biitha, Taasisi ya Hija na Taasisi ya Mashahidi, zitekeleze vilivyo na zifuatilie kwa uzito mkubwa majukumu yao kuhusiana na tukio kubwa la Mina.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Qadhi Asgar, mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) katika masuala ya Hija na Ziara ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kuwakumbuka mashahidi wa Septemba 8, 1978, na pia mashahidi wa Ijumaa ya umwagaji damu huko Makkah iliyotokea mwaka 1366 Hijria Shamsia (Agosti 2, 1987) na mashahidi wa Hija ya mwaka jana na kusema kuwa, maafa mawili makubwa ya Mina na lile la ndani ya Masjidul Haram, yaliigeuza furaha ya Hija kuwa msiba na kuwatumbukiza watu na familia zao kwenye majonzi makubwa.
Hujjatul Islam Walmuslimin Qadhi Asgar amegusia pia namna Wasaudia wanavyokwamisha juhudi za kuundwa kamati ya kutafuta ukweli kuhusu maafa hayo na kusema kuwa, Taasisi ya Biitha ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Taasisi ya Hija ya Iran zimekusanya ushahidi mbali mbali uliotolewa kuhusiana na maafa hayo na kwamba imeshirikiana na wanasheria kugundua njia za kulifuatilia jambo hilo katika taasisi za kisheria za kimataifa na kamwe hazitaruhusu suala la Mina lisahauliwe.
Naye Hujjatul Islam Walmuslimin Shahidi Mahallati, mwakilishi wa Fakihi Mtawala ambaye pia ni mkuu wa Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Kujitolea katika Njia ya Haki ametoa ripoti fupi kuhusiana na kazi na hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo kuhusu matukio ya Mina na Masjidul Haram na kusema: Maafa ya kutisha na kutia majonzi ya Mina yametokea kutokana na uendeshaji mbaya na uanagenzi wa ukoo wa Aal Saud.

3528593


captcha