IQNA

Mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika masuala ya Hija na Ziara za Kidini Iran

Nchi za Kiislamu zishirikiane zaidi katika suala la Hija

12:22 - July 21, 2016
Habari ID: 3470467
Mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika masuala ya Hija na Ziara za Kidini Iran amesisitiza kuhusu Diplomasia ya Hija baina ya nchi zote za Kiislamu hasa Iran na Pakistan.

Hujjatul Islam wal Muslimin Sayyed Ali Qadhi Askar Mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika masuala ya Hija na Ziara za Kidini nchini Iran, akiwa safarini  Pakistan Siku ya Jumatano, alikutana na kufnaya mazungumzo na Mohammad Yusuf, Waziri wa Masuala ya Kidini nchini humo.

Sheikh Qadhi Askar alisema: "Kwa kuzingatia matukio ya kusikitisha mwaka jana katika siku za Hija huko Saudi Arabia, kunahisika haja ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa nchi katika suala la Hija."

Sheikh Qadi Askar ameashiria idadi kubwa ya Waislamu wa Pakistan wanaokuja Iran kwa ajili ya ziara za kidini katika maeneo matakatifu nchini au wakiwa njiani kuelekea maeneo matakatifu Iraq na Syria, kuna haja ya kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili kwa lengo la kurahisisha safari hizo.

Mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika masuala ya Hija na Ziara za Kidini pia ameashiria suala la chuki dhidi ya Uislamu na kubainisha masikitiko yake kuhusu njama za baadhi ya madola makubwa ambayo yanaibua wimbi la chuki dhidi ya Uislamu duniani ambapo amependekezea waziri wa masuala ya kidini Pakistan njia za kukabiliana na tatizo hilo.

Waziri wa masuala ya kidini Pakistan kwa upande wake ameutaja uhusiano wa Iran na Pakistan kuwa wa kirafiki sana na kuongeza kuwa: "Ibada ya Hija ni nembo ya Umoja wa Umma wa Kiislamu na Pakistan iko tayari kwa ajili ya kuimarisha umoja na ushirikiano na Iran."

Kwingineko Sheikh Qadhi Askar akiwa Pakistan pia amekutana na shakhsia wa kidini na kisiasa  nchini Pakistan na kusema: "Taifa na serikali ya Iran inasisitiza daima kuhusu kuimarishwa uhusiano wa Iran na Pakistan."

Aidha amebainisha kuhusu masuala yaliyopo baina ya Iran na Saudi Arabia na kusema: "Iran inataka mgogoro baina yake na Saudia utatuliwe kwa mazungumzo lakini Saudia imekataa kufuata mkondo huu."

Kwa kuzingatia yaliyojiri katika ibada ya Hija mwaka jana, wakuu wa Saudia wametumia sababu za kisiasa kuwazuia Mahujaji wa Iran kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu.

Katika ibada ya Hija mwaka jana, mnamo tarehe 24 Septemba mwaka 2015, kufuatia uzembe wa utawala wa Aal Saud, kulijiri msongamano mkubwa wa Mahujaji katika eneo la Mina ambapo maelfu walipoteza maisha wakiwemo Mahujaji 461 kutoka Iran.

Ikiwa ni takribani mwaka moja tokea kuuawa shahidi maelfu ya Mahujaji wa Nyumba ya Allah SWT katika maafa ya Mina, na pamoja na ahadi zilizotolewa na utawala wa Saudia, hadi sasa hakuna melezo yoyote yaliyotolewa kwa nchi za Kiislamu kuhusu maafa hayo ya kuogofya.


3516355

captcha