IQNA

Matukio yanayohusu Palestina

Afisa wa Jeshi la Marekani kabla ya kujichoma alifichua siri ya Marekani kuhusika na mauaji ya kimbari Gaza

17:50 - February 29, 2024
Habari ID: 3478433
IQNA-Gazeti la New York Post limechapisha maelezo mapya kuhusu mwanajeshi wa Jeshi la Anga la Marekani, Aaron Bushnell ambaye alijichoma moto mbele ya ubalozi wa Israel mjini Washington akipinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Gaza, na kumnukuu rafiki yake akisema kwamba Bushnell alimwambia ameona taarifa za siri zinazoonyesha ushiriki wa "vikosi vya jeshi Marekani katika kuua idadi kubwa ya Wapalestina.”

Kulingana na maelezo ya rafiki wa karibu wa rubani huyo wa Marekani ambaye jina lake halikuchapisha, Bushnell (25) alimfahamisha kwamba, alikuwa na kibali kinachomruhusu kutazama data za ujasusi za jeshi la Marekani zilizoainishwa kama " siri kuu."

Bushnell alikuwa akihudumu katika Kitengo cha 70 cha Ujasusi, Ufuatiliaji na Upelelezi wa Jeshi la Anga la Marekani, ambako inasemekana alifanya kazi kama "Fundi wa Huduma za Ubunifu."

Rafiki yake, ambaye gazeti la New York Post limethibitisha kuwa alikuwa na uhusiano mkubwa na Bushnell, amesema, "kazi yake halisi ilihusisha kuchakata data za kijasusi, ambazo baadhi zilihusiana na mzozo wa Israel huko Gaza."

Ameeleza kuwa Bushnell alimpigia simu usiku wa Jumamosi, Februari 24 - yaani, saa chache kabla ya kujichoma moto Jumapili mchana - na kumwambia kwamba baadhi ya habari alizoziona zilionyesha kuwa "jeshi la Marekani linahusika katika operesheni za mauaji ya kimbari zinazoendelea Palestina."

Aliendelea kusema kwamba: "Aliniambia Marekani imetuma vikosi vya nchi kavu, na kwamba wanaua idadi kubwa ya Wapalestina."

Pia ameeleza kuwa Bushnell alizungumza kuhusu wanajeshi wa Marekani wanaopigana kwenye mahandaki yanayotumiwa na makundi ya mapambano ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Jumatatu iliyopita, Aaron Bushnell alielekea katika ubalozi wa Israel mjini Washington ambako alijimwagia petroli kichwani na nguoni na kujichoma moto huku akikariri kwa sauti kubwa: “Palestina Huru, Palestina Huru” hadi alipokata pumzi. Rubani huyo shujaa mtetezi wa Wapalestina ambaye alisema kwa sauti kubwa kwamba hataki kushiriki tena katika mauaji ya kimbari, aliaga dunia baadaye. 

Tamko la Hamas kuhusu Bushnell

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema serikali ya Marekani inabeba dhima ya kifo cha mwanajeshi wa nchi hiyo aliyejichoma moto nje ya Ubalozi wa Israel huko Washington akipinga uungaji mkono wa serikali ya Rais Joe Biden kwa mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel huko Ukanda wa Gaza.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema: "Utawala wa Biden unabeba dhima kamili ya kifo cha rubani wa Jeshi la Marekani, Aaron Bushnell, kutokana na sera zake zinazounga mkono mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni ya kuwaangamiza watu wa Palestina."

Hamas imeeleza kuwa: "Bushnell "ametoa mhanga maisha yake kwa shabaha ya kumulika mauaji ya kimbari na ya kizazi yanayofanywa na Wazayuni dhidi ya watu wetu katika Ukanda wa Gaza."

Hamas pia imetuma salamu za rambirambi na mshikamano wake kwa familia na marafiki wa rubani wa huyo wa Marekani, Aaron Bushnell.

Taarifa ya Hamas imesisitiza kuwa, rubani Aaron Bushnell amebakisha hai jina lake kama mtetezi wa maadili ya kibinadamu na mpinzani wa ukandamizaji dhidi ya watu wa Palestina ambao wanaendelea kuteseka kwa sababu ya utawala wa Marekani na sera zake za kidhalimu; kama ilivyokuwa kwa mwanaharakati wa Marekani, Rachel Corrie, ambaye alisagwasagwa na tingatinga la Israel huko Rafah mnamo 2003 (akiwatetea Wapalestina).

Hamas imeongeza kuwa, Rafah ni mji uleule ambao Bushnell amesabilia maisha yake ili kuishinikiza serikali ya nchi yake "izuie jeshi la wahalifu la Israel kuushambulia na kufanya mauaji na ukiukaji wa sheria huko."

Harakati ya Hamas imeendelea kwa kusema: "Rubani shujaa Aaron Bushnell atabaki milele katika kumbukumbu ya watu wetu wa Palestina na watu huru duniani, na ni ishara ya roho ya mshikamano wa kibinadamu wa kimataifa na watu wetu na mapambano yao ya kupigania haki."

Jana, Jumatatu, Aaron Bushnell alielekea katika ubalozi wa Israel mjini Washington. ambako alijimwagia petroli kichwani na nguoni na kujichoma moto huku akikariri kwa sauti kubwa: “Palestina Huru, Palestina Huru” hadi alipokata pumzi. Rubani huyo shujaa mtetezi wa Wapalestina aliaga dunia baadaye. 

Biden akiri tena kuwa binafsi ni Mzayuni

Kwa mara nyingine tena rais wa Marekani amejigamba kuwa yeye ni Mzayuni na anaunga mkono jinai za Israel licha ya idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi hivi sasa kutokana na jinai za utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Gaza, kupindukia 30,000.

Joe Biden, ambaye serikali yake inachangia kikamilifu jinai za Israel kwa njia mbalimbali zikiwemo za msaada kamili wa kijeshi, kifedha na kidiplomasia tangu jinai hizo zilipoanza tarehe 7 Oktoba 2023, dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, amejigamba kwenye mahojiano ya televisheni kwamba yeye ni Mzayuni na ataendelea kuunga mkono jinai hizo hadi pale HAMAS itakapofutwa kabisa. 

Amesema kwa majivuno kwamba: "Ili kuwa Mzayuni, si lazima uwe Myahudi. Mimi ni Mzayuni. Lau kama Israel isingelikuwepo, hivi sasa asingekuwepo Myahudi yeyote duniani."

Utawala wa kibeberu wa Marekani ulitangaza mshikamano wake na utawala wa Kizayuni mara baada ya Israel kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba mwaka jana. 

Katika siku za mwishoni mwa mwezi Disemba 2023 pia, Biden aliwakaribisha Mayahudi katika Ikulu ya White House na kusema: Marekani itaendelea kutuma misaada ya kijeshi kwa Israel.

Pia amesema: Wakati miaka michache iliyopita niliposema kuwa si lazima kuwa Myahudi ili uwe Mzayuni, nilishutumiwa sana, lakini mimi ni Mzayuni. Tukiweka kando tofauti zetu na Waziri Mkuu wa Israel, niseme ukweli, ahadi yangu ya kuweko dola la Kiyahudi haiyumbi"

Dunia nzima inaendelea kulaani jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina, lakini rais wa Marekani anaona fakhari kutangaza hadharani kuwa anaunga mkono kikamilifu jinai hizo.

Habari zinazohusiana
captcha