IQNA

Hujuma ya Magaidi wa Al Shabab dhidi ya vituo vya jeshi la Somalia

15:04 - February 20, 2020
Habari ID: 3472488
TEHRAN (IQNA) - Magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Shabab wametekeleza mashambulizi dhidi ya vituo viwli vya Jeshi la Somalia katika eneo la Lower Shabelle na kuua askari wasiopungua wanne.

Kwa mujibu wa taarifa, shambulizi la kwanza lilijiri Jumatano katika kituo cha kijeshi cha el-Salini yapata kiliomita 55 kusini magharibi mwa mji mkuu, Mogadishu.

Msemaji wa Jeshi la Somalia Ismail Mukhtar amenukuliwa akisema wanajeshi wamefanikiwa kuwaua magaidi tisa katika shambulio hilo.  Naye Kanali Hassan Mohamed Abukar amethibitisha kuwa wanajeshi wasiopungua wanne wameuawa katika hujuma hiyo.

Shambulizi la pili pia limejiri Jumatano katika mji wa Qoryoley katika kituo cha kijeshi ambacho kinatumia na askari wa Jeshi la Somalia na wale wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika (AMISOM).  Mji huo wa Qoryoley uko umbali wa kilimota 120 kutoka Mogadishu na ni maarufu kwa shughuli za kilimo.

Gavana wa Lower Shabelle Ibrahim Adan amewaambia waandishi habari kuwa magaidi watatu wa Al-Shabab wameuawa katika kituo hicho na kwamba hakuna askari yeyote wa Jeshi la Somalia au AMISOM aliyeuawa.

Jeshi la Somalia limesema limetekeleza oparesheni kadhaa katika eneo hilo na kukomboa vijiji vinne ambavyo vilikuwa vimetkewa na al-Shabaab.

Magaidi wa al-Shabaab wamekiri kuhusika na hujuma hizo mbili na kudai kuwa wameua askari 20 na kupora zana za kivita.

Kundi la kigaidi la al-Shabab lilianza hujuma zake nchini Somalia mwaka 2007 na limekuwa likiendesha ugaidi katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine ya Somalia na pia katika nchi jirani ya Kenya. Magaidi hao walitumuliwa Mogadishu Agosti 2011 katika operesheni iliyofanywa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM, lakini limekuwa likifanya mashamabulizi ya kuvizia mara kwa mara.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wa al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM wanaokadiriwa kufikia 21,000 wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 ili kujaribu kukabiliana na magaidi wa al-Shabab. Hatahivyo pamoja na vitihada hizo za kimataifa, magaidi wa al-Shabab wanaendelea kutekeelza hujuma Somalia na nchi jirani ya Kenya.

3470696

captcha