IQNA

Waislamu wa kabila la Rohingya wahangaika baharini

19:31 - May 19, 2015
Habari ID: 3305556
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameelezea wasiwasi wake kuhusu hatma ya wakimbizi na wahamiaji, wengi wao Waislamu wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar, walioachwa kwenye Bahari ya Andaman na Lango la Malakka, kati ya Myanmar, Thailand na Malaysia.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu huyo amenukuliwa akiwasihi viongozi wa ukanda wa Asia Kusini Mashariki kuwaokoa wahamiaji hao na kutowakatalia kushuka. Katika siku chache zilizopita, Ban ameongea na Waziri Mkuu wa Malaysia na Thailand, huku Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Bangladesh na Naibu Waziri wa Masuala ya Kimataifa wa Indonesia. Katika mazungumzo yao, wamesisitiza umuhimu wa kulinda maisha ya binadamu na kuheshimu sheria ya kimataifa. Aidha wamesisitiza umuhimu wa kukubali wahamiaji hao wateremke kwenye muda mwafaka. Aghalabu ya wahimiaji hao ni Waislamu wa kabila la Rohinyga wanaokandamizwa na kuteswa nchini Myanmar na ambao sasa wanakimbilia nchi jirani ili kuokoa maisha yao. Katika upande mwingine Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imetoa wito wa kusaidiwa maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na hujuma na mauaji yanayofanywa dhidi yao na Mabudha.

Iyad Amin Madani, Katibu Mkuu wa OIC ameitaka jamii ya kimataifa kutafuta njia mwafaka za kushugulikia tatizo la Waislamu hao ambao wanatanga tanga katika maji ya eneo la kusini mashariki mwa Asia. Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu amesema kuwa, serikali ya Myanmar inapaswa kuruhusu kuingizwa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Waislamu hao. Serikali ya Myamnar inawatambua Waislamu wa Rohingya kuwa ni wahajiri haramu kutoka nchi jirani ya Bangladesh na imekuwa ikikataa kuwapatia uraia kamili.

Serikali ya Myanmar imekuwa ikikosolewa na mashirika ya haki za binadamu kwa kushindwa kuwalinda Waislamu wa Rohingya wanaokabiliwa na unyanyasaji na mauaji yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali. Maelfu ya Waislamu wameuawa nchini Myanmar na wengine wengi wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na hujuma hizo.../mh

3305475

captcha