IQNA

Haram ya Imam Ridha AS katika mkesha wa kukumbuka siku yake ya kuzaliwa

TEHRAN (IQNA)- Makumi ya maelefu ya wafanyaziara kutoka Iran na nchi za kigeni wako katika mji Mtakatifu wa Mashhad kwa ajili ya kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Ridha AS

Ikumbukwe kuwa, Siku kama ya leo miaka 1295 iliyopita, sawa na tarehe 11 Dhulqaad mwaka 148 Hijria, alizaliwa Imam Ali bin Mussa Ridha (as), mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (as) katika mji wa Madina. Imam Ridha alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu mara baada ya kufariki dunia baba yake Imam Mussa al-Kadhim AS, mnamo mwaka 183 Hijiria. Shakhsia huyo alikuwa mbora zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu wakati wa zama zake. Kwa minajili hiyo, Ma'amun Khalifa wa Kiabbasi alijaribu kumpatia wadhifa Imam Ridha (as) kwa shabaha ya kuimarisha nafasi yake na wakati huo huo kumdhibiti Imam. Imam Ridha AS alikubali pendekezo hilo kwa kulazimishwa na kwa mashinikizo ya utawala wa Ma'amun. Mtukufu huyo aliwaeleza Waislamu wote, wakiwemo watu wa eneo la Khorasan, ukweli wa mambo ulivyo, na kuwaathiri mno wananchi kuhusiana na uhakika wa Ahlul-Bayt wa Mtume AS.