IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kuna haja ya kusimama kidete kukabiliana na njama za Saudia, Imrati za kuigawanya Yemen

13:14 - August 14, 2019
Habari ID: 3472083
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, Saudi Arabia na Imarati zinataka kuigawanya Yemen; na akasisitiza kwamba: Inalazimu kusimama na kukabiliana kwa nguvu zote na njama hiyo na kuunga mkono Yemen moja, iliyoungana na yenye ardhi yake yote kamili.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ametoa sisitizo hilo Jumanne mjini Tehran alipotembelewa na ujumbe wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ulioko safarini nchini Iran.

Katika mazungumzo hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amepongeza na kusifu imani, kusimama imara, urazini na moyo wa jihadi wa wananchi wa Yemen katika kukabiliana na uvamizi mkubwa na wa kinyama wa Saudia, Imarati na waungaji mkono wao; na akasisitiza kwamba: Ili kulinda umoja wa ardhi yote ya Yemen, kwa kuzingatia imani na itikadi za kidini na za makabila tofauti ya nchi hiyo, kuna haja ya kufanyika mazungumzo baina ya Wayemeni wenyewe.

Ayatullah Khamenei ameongezea kwa kusema: Kutokana na ustaarabu mkubwa na wa kihistoria walionao watu wa Yemen, na kwa moyo wa jihadi na kusimama imara walioonyesha katika muda huu wa miaka mitano, watakuwa na mustakabali mzuri; na wataweza kuunda serikali imara na kupata maendeleo kupitia serikali yao hiyo.

Kiongozi Muadhamu ameashiria pia misimamo dhidi ya Marekani na dhidi ya Magharibi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasisitiza kwamba: Misimamo hii haitokani na taasubi, bali inatokana na uhalisia wa mambo na utendaji wa viongozi wa Marekani na Magharibi, ambao kwa kujifanya kidhahiri kuwa na utu, ustaarabu na maadili wanatenda jinai mbaya kabisa.

Ayatullah Khamenei amesema: Kutoshughulishwa Ulimwengu wa Magharibi na jinai zinazofanywa Yemen na Palestna ni mfano mmojawapo wa hali halisi ya dunia ya leo.

Awali ya mazungumzo hayo, Muhammad Abdussalam, msemaji wa harakati ya Ansarullah alimkabidhi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu barua kutoka kwa kiongozi wa harakati hiyo Sayyed Abdulmalik Badruddin na kumueleza kwamba: Wananchi wa Yemen, ambao wako katika kipindi kigumu mno, wamesimama imara kukabiliana na uvamizi wa nchi 17 wakiwa mikono mitupu, lakini wakitegemea imani na msimamo wao thabiti.

Abdussalam ameongezea kwa kumhutubu Kiongozi Muadhamu: Tunakupa ahadi kwamba, wananchi wa Yemen, wakiwa wameshikamana mithili ya mkono mmoja, wataendeleza muqawama na istiqama kukabiliana na uvamizi wa kidhalimu, hadi ushindi kamili.

3834734

captcha