IQNA

Balozi wa Palestina Tehran

Ardhi ya Palestina Lazima Irejee kwa Wapalestina

10:41 - July 09, 2019
Habari ID: 3472037
TEHRAN (IQNA) - Balozi wa Palestina nchini Iran amesema utawala haramu wa Israel unapaswa kusitisha ukaliaji mabavu ardhi za Palestina huku akisisitiza kuwa, Palestina ni lazime irejee kwa Wapalestina.

Akizungumza mjini Tehran katika kikao cha kujadili 'Nukta za Muamala wa Karne' Balozi wa Palestina nchini Iran Salah al-Zawawi amesema Wapalestina wote wanapinga 'Muamala wa Karne' ambao ni njama ya pamoja ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kikao hicho kilifanyika katika makao makuu ya Shirila la Habari la Qur'ani la Kimataifa siku ya Jumatatu na kuhudhuriwa pia na Hussein Sheikhul Islam, mwanadiplomasia mkongwe wa Iran ambaye pia ni mshauri wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu.
Zawawi amesema 'Muamala wa Karne' ni sehemu ya njama ya kuunda 'Israeli Kuu', kwa kupora ardhi zote za Palestina, lakini hakuna kundi lolote la Palestina linalounga mkono mpango huo.
Akijibu swali ni kwa nini sehemu ya kwanza ya 'Muamala wa Karne' imeangazia masuala ya kiuchumi, amesema wakuu wa Marekani wana dhana potovu kuwa, kwa kuwapa pesa Wapalestina wanaokumbwa na masaibu ya kiuchumi, wangeweza kuwafanya wasitishe harakati zao za ukombozi.
Aidha ametupilia mbali uwezekano wa suluhisho la kisiasa katika kadhia ya Palestina na kusema kuzungumza kuhusu amani na Israel ni ndoto isiyoweza kutimia.
Kwingineko katika matamshi yake, Zawawi ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na msimamo wake imara wa kuunga mkono ukombozi wa Palestina. Amesema tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Imam Khomeini MA, Iran imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono Palestina na kukabiliana na njama za Israel. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi pekee ya Kiislamu inayosimama kidete kukabiliana na njama za Israel.
Kikao cha siku mbili cha mpango wa 'Muamala wa Karne' kilifanyika Juni 25-26 huko Manama, mji mkuu wa Bahrain huku kukiwa na maandaman na malalamiko makubwa ya raia wa nchi za Asia Magharibi dhidi yake.
Kikao hicho kinadaiwa kufanyika kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa kigeni kwa maslahi ya Wapalestina. Marekani ambayo imeandaa na kusimamia kikao hicho, inafanya njama za kutumia ibara za hadaa za kiuchumi na uwekezaji kwa ajili ya kupunguza makali ya malalamiko na upinzani wa Wapalestina dhidi ya mpango huo.
Nukta muhimu hapa ni kwamba nafsi ya kufanyika kikao hicho cha Manama ni batili, kwa sababu waandaaji wake wamedai kwamba kimefanyika kwa ajili ya maslahi ya Palestina katika hali ambayo hakuna hata kundi moja la Palestina lililoshiriki kikao hicho. Makundi yote ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina yalipinga vikali kikao hicho na kusisitiza kuwa nchi za Kiarabu zilizotuma wajumbe wao katika kikao hicho zimelisaliti taifa la Palestina.

http://iqna.ir/fa/news/3825459

captcha