IQNA

Wasomaji Qur’ani Wairani kutembelea nchi saba ikiwemo Tanzania katika Wiki ya Umoja wa Kiislamu

11:30 - December 01, 2017
Habari ID: 3471290
TEHRAN (IQNA)-Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatuma ujumbe wa wasomaji Qur’ani katika nchi saba duniani kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu na Maulidi ya Mtume Muhammad SAW.

Kwa mujibu wa Bw. Mohammad Taqi Mirzajani, mkurugenzi mtendaji wa Baraza Kuu la Qur’ani nchini Iran, kila kundi litakuwa na qarii wa Qur’ani Tukufu, Hafidh wa Qur’ani na pia kundi la qaswida.

Amesema nchi ambazo zitatembelea wanaharakati hao wa Qur’ani kutoka Iran ni pamoja na Afrika Kusini, Senegal, Tanzania, Sri Lanka, Pakistan, Afghanistan na Russia.

Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shiia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini MA Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

3668256

captcha