IQNA

Asilimu baada ya mwenye chuki dhidi ya Uislamu kuwataka watu wasome Qur'ani

12:01 - October 04, 2017
Habari ID: 3471204
TEHRAN (IQNA)-Mtu moja aliyemsikia mwanachama wa chama chenye chuki dhidi ya Uislamu akiwataka watu waisome Qur'ani kwa lengo la kuikosoa alifuata ushauri huo lakini kinyume na ilivyotarajiwa, alipata muongozo na kusilimu.

Hivi karibuni, Tommy Robinson, kiongozi wa zamani wa chama cha wazungu wenye misimamo mikali na wanaouchukia Uislamu nchini Uingereza kinachojulikana kama English Defense League (EDL) akizungumza katika televisheni alikuwa ameshika mkononi tarjama ya Qur'ani Tukufu na kuwataka watu waisome kwa lengo la kuupiga vita Uislamu. Kati ya waliokuwa wakisikiliza mahojiano hayo ni Christos Onassis ambaye anasema: "Alitutaka tusome Qur'ani akidhani kuwa watu wakisoma kitabu hicho watauchukia Uislamu. Nilifuata ushauri huo na kusoma Qur'ani na hapo nikaweza kutambua ukweli na haki na kwa njia hiyo nikaukumbatia Uislamu." Hivi sasa Christos Onassis amebadilisha jina lake na anajulikana kama Abdul-Bari Onassi. Katika ujumbe kupitia akaunti yake ya Twitter, Onassis pia amesema amekuwa akisoma jumbe za Twitter za Robinson za kutaka watu wasome Qur'ani na kuongeza kuwa baada ya kusoma aliamua kutamka Shahada yaani "Hakuna Mola apasaye kuabudiwa isipokuwa Allah na Muhammad ni Mjumbe Wake."

Anasema Robinson hakuwa anafahamu anachokizungumza na wala hakuwa na uelewa wowote kuhusu tafsiri ya Qur'ani Tukufu.

Wakati akihojiwa katika televisheni ya ITV ya Uingereza, Robinson alikuwa ameshika mkononi nakala ya tarjama ya Qur'ani Tukufu huku akidai kuwa kitabu hicho kitakatifu kinachochea mauaji. Wakati alipobanwa na mtangazaji Piers Morgan, Tommy alijibu kwa kuuliza, "Wewe Umekisoma kitabu hiki?"

Baada ya kipindi hicho, idadi kubwa ya watu wasiokuwa Waislamu walitaka kusoma tarajama ya Kiingereza ya Qur'ani Tukufu.

Pamoja na kuwepo chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi na maeneo mengine duniani, kunashuhudiwa wimbi la watu wengi wakiendelea kusilimu. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na taasisi ya PEW, Uislamu ndio dini inayoenyea kwa kasi zaidi duniani na moja ya sababu zake ni kutokana na Wakristo wengi kusilimu.

3464074

captcha